Social Icons

Pages

Tuesday, June 15, 2010

Love like Butterfly

PENZI KAMA KIPEPEO!(Dedicated to Princess Lumy)


Kipepeo ana fumbo, mtazame kwa makini,

Rangi yake na marembo, uyapige darubini,

Amesheheni mapambo, ya kupendeza machoni

Penzi kama kipepeo.

Mtima huwa mwepesi, penzi liwapo moyoni,

Kipepeo muasisi, hewani hana uzani,

Kwa mbio kama farasi, midundo ya kifuani,

Penzi kama kipepeo.

Mapenzi hutupa mbawa, tuweze ruka angani,

Nyoyo zetu zikapowa, tukaishi kwa amani,

Hata tujapo kosewa, msamaha kutohini,

Penzi kama kipepeo.



Hutusafirisha mbali, tufike ughaibuni,

Wana rangi mbali mbali, vipepeo msituni,

Kunao wa bei ghali, na wa gharama ya chini,

Penzi kama kipepeo.

Ukimshika imara, atakufa masikini

Iwe kwako ni hasara, dhiki nyingi na huzuni

Uhuru iwe ni sera, usimfungie ndani,

Penzi kama kipepeo.

Penzi ukilikimbiza, hulipati ikhiwani,

daima litakupeza, ubaki kulitamani,

Kijitia mapuuza, atatua mwako begani,

Penzi kama kipepeo.


Kimanga Bismarck.

"Malenga muadilfu"

© 2010.

No comments: